Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TANZANIA NA KENYA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA YA NAFAKA

Imewekwa: 29 Jan, 2026
TANZANIA NA KENYA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA YA NAFAKA

Tanzania na Kenya zimedhamiria kuimarisha uhusiano wa kibiashara katika mnyororo wa thamani wa nafaka, hususan mahindi meupe na mpunga, kufuatia mazungumzo kati ya Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Tanzania, na Dkt. Kipronoh Ronoh, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Kenya, yaliyofanyika tarehe 28 Januari 2026 jijini Nairobi, nchini Kenya.

Katibu Mkuu Mweli amesema kuwa Tanzania ina uzalishaji wa kutosha wa mahindi ambapo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) kwa sasa ina akiba ya zaidi ya tani 500,000 za mahindi na mpunga.  Hivyo, ameeleza kuwa Tanzania iko tayari kuendelea kufanya biashara ya mahindi na Kenya kulingana na mahitaji ya soko la nchi hiyo.

Katika hatua nyingine, ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu Mweli umefanya vikao na uongozi pamoja na timu za kitaalamu kutoka Wizara ya Kilimo yaKenya, Agriculture and Food Authority (AFA) na Cereal Growers Association (CGA), na kujadili mikakati ya kuimarisha biashara endelevu ya mazao ya nafaka, kuimarisha akiba ya chakula ya kimkakati, pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wengine katika ujumbe wa Tanzania ni Balozi John Ulanga, Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya NFRA, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba.