UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO MOROGORO WAFIKIA VIJIJI 130
Zoezi la ukusanyaji wa sampuli za udongo kwa ajili ya upimaji wa Afya ya udongo, mkoani Morogoro limeendelea ambapo hadi sasa jumla ya vijiji 130 katika kata 30 za halmashauri ya Wilaya ya Mvomero vimefikiwa; huku upimaji ukiendelea katika Halmashauri ya Wilaya Malinyi, Ulanga, Ifakara, Morogoro vijijjini, Kilosa na Gairo
Zoezi hii ni utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara ya Kilimo kupitia Programu ya Mifumo
Himilivu ya chakula (TFSRP) kiashiria namba 7, ambapo kwa mkoa wa Morogoro wataalamu hao wamelenga kukusanya jumla ya sampuli 8640 ikijumuisha sampuli 7200 kutoka katika mashimo mafupi na sampuli 1440 kutoka katika mashimo marefu (profile pits)
"Tunahitaji watu mliojizatiti kama ninyi mtuambie cha kufanya, mnapokwenda Malinyi mjue kule kuna mpango wa eneo hilo na mkoa kwa ujumla wa kuzalisha takribani tani Milioni 2 za mpunga, ili tuwe wazalishaji wa kuwaondoa watu katika umaskini sayansi hii ni muhimu sana kwetu,” amesema Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Nao baadhi ya wakulima waliofikiwa na zoezi hili katika vijiji mbalimbali mkoani humo ikiwemo kijiji cha Mziha, Kanga, Lukenge pamoja na vijiji vingine, wamewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu mara wanapokua katika maeneo yao ili kufanikisha utekelezaji wa zoezi hili.
"Tunatamani kujua tunalima vipi ili tuvune mazao mengi zaidi, na kulingana na maelezo ya hawa wataalamu naona ni bora tukawaunga mkono na kuwapa nafasi ili tujue tutumie mbolea gani katika kilimo, tumekua tukinununua mbolea na mbegu za kisasa dukani na hata tukipanda tunapata wastani, tungependa kupata zaidi", amesema Bi. Mwajabu Ali ambaye ni mkulima katika kijiji cha Mziha kata ya Mziha, wilayani Mvomero.
Zoezi hili pia linaendelea katika mikoa ya Tanga, Pwani, Lindi naTabora na mara baada ya kukamilika litawezesha uandaaji wa ramani ya afya ya udongo kidigitali itakayotoa dira kuhusu zao lipi linastahimili udongo husika, aina ya mbolea pamoja na zana za kilimo zinazoendana na hali ya udongo.