Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO: MAGEUZI YA KILIMO YANACHOCHEA UCHUMI WA TAIFA

Imewekwa: 16 Sep, 2026
CHONGOLO:  MAGEUZI YA KILIMO YANACHOCHEA UCHUMI WA TAIFA

Mageuzi ya kilimo nchini yameelezwa kuwa nguzo muhimu ya kukuza uchumi kwa kuinua kipato cha wakulima na kuongeza ustawi wa Taifa.

Amesema hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) tarehe 09 Septemba 2026 wakati akizindua kiwanda cha kisasa cha kuchakata mbegu cha Kampuni ya Seed Co Tanzania kilichopo mkoani Arusha. 

Amefafanua kuwa uwepo wa kiwanda hicho kielelezo cha ushirikiano thabiti kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) katika kuchochea mageuzi ya kweli ya kiuchumi kupitia Sekta ya Kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa.  Aidha, Waziri Chongolo ametoa wito kwa uongozi wa kampuni hiyo kuhakikisha mbegu zinawafikia wakulima kwa urahisi, sambamba na kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi kwa kushirikiana na maafisa ugani. “Kilimo ni biashara, na sasa kazi inaendelea!”, amesisitiza Waziri Chongolo. 

Akizungumza zaidi katika hafla hiyo, Waziri Chongolo ameeleza kuwa chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kuongeza bajeti ya kilimo na kusukuma mbele Ajenda 10/30 inayolenga kukuza Sekta hiyo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Programu nyingine kama Jenga Kesho iliyobora (Building a Better Tomorrow - BBT) nazo zinaendelea kuwajengea uwezo wa kibiashara vijana na wanawake ili kulifanya Taifa kujitegemea kwa chakula.

Uwekezaji wa Seed Co unatarajiwa kupunguza utegemezi wa kuagiza mbegu kutoka nje ya nchi, huku ukihakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa wakati na kwa gharama nafuu.  Kiwanda hicho pia kinayarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania na kufungua milango ya fursa kupitia mifumo ya kilimo cha mkataba (outgrower schemes) kwa wakulima wa ndani.

Katika kuimarisha tasnia ya mbegu, Serikali kupitia taasisi za Kilimo za TARI, ASA, na TOSCI imejipanga kuhakikisha miundombinu ya utafiti na mifumo ya udhibiti wa ubora kwa njia za kisasa na kidijitali.  Hatua hii inaweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu (hub) cha kusambaza mbegu bora katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.