CHONGOLO: TANZANIA IKO TAYARI KUILISHA KIBIASHARA KONGO DRC
Serikali ya Tanzania imesema iko tayari kuingia mazungumzo katika nyanja mbalimbali za kibiashara na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiwemo biashara ya chakula.
Amesema hayo Waziri Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo wakati wa Mkutano wake na Bw. Tony Bandio Munongo, Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika masuala ya Uchumi na Uwekezaji tarehe 13 Machi 2026, mkoani Dodoma.
Washiriki wengine katika Mkutano ni pamoja na Bw. Fredy Matamba, Mshauri Msaidizi wa Rais wa Kongo DRC katika masuala ya Uchumi na Uwekezaji ukiwemo ujumbe wa watu tisa kutoka Serikali ya Kongo DRC; Prof. Peter L. M. Msoffe, Naibu Katibu Mkuu (Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula); Dkt. Andrew Komba, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na timu yake ya wataalamu.
Ujumbe huo upo nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awali wa mkutano wa uwili kati ya Waziri Chongolo na Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Kongo DRC, Mhe. Muhindo Nzangi Butondo walipokutana nchini Ujerumani pembezoni mwa Mkutano wa 18 wa Kimataifa wa Chakula na Kilimo (GFFA).
Ziara yao nchini itahusisha kujionea ubora wa mahindi yanayozalishwa na kuhifadhiwa chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), pamoja na kujifunza na kujadiliana kuhusu taratibu za ununuzi na mifumo ya usafirishaji wa mahindi hayo kwenda Kongo DRC.
Wakati wa mazungumzo yao, Waziri Chongolo amekaribisha ushirikiano utakaongeza wigo wa biashara katika mazao ya chakula, masoko, usafirishaji na maeneo mengine ya kibiashara. Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni utekelezaji wa maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha chakula cha kutosha na ziada ili kulisha kibiashara nchi za ukanda wa EAC na SADC.