Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

DKT. NINDI AONGOZA KIKAO CHA UHAMASISHAJI MATUMIZI YA MBOLEA MBEYA

Imewekwa: 04 Oct, 2025
DKT. NINDI AONGOZA KIKAO CHA UHAMASISHAJI MATUMIZI YA MBOLEA MBEYA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi, ameongoza kikao maalum katika Bonde la Uyole, Mbeya, tarehe 03 Septemba 2025 kilicholenga uhamasishaji wa matumizi ya Mbolea. Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa kilimo na wakulima, jambo lililoonesha mshikamano mkubwa katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.

Dkt. Nindi, katika hotuba yake, amewashukuru wakulima kwa mwitikio wao mkubwa na kusisitiza umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la mkulima ili kunufaika na ruzuku za Serikali. Pia alielekeza kuanzishwa kwa mashamba darasa kwa kushirikiana na wadau, pamoja na kuhakikisha kuwa huduma za ugani zinawafikia wakulima mara kwa 

Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Rodrick Mpogolo amesema Mkoa wa Mbeya ni kitovu cha kilimo kwa Nyanda za Juu Kusini na kubainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia upimaji wa afya ya udongo na kuongeza tija kwa wakulima. Ameomgeza kuwa fursa zilizopo, hususan kwenye kilimo cha Mpunga, Chai, Parachichi na Kokoa, zinaweza kuongeza uchumi wa wakulima endapo changamoto ndogo zilizopo zitatatuliwa kwa ushirikiano.

Wakulima wa Skimu ya Iganjo walioshiriki kikao hicho wameipongeza Serikali kwa juhudi zake, huku wakiomba upatikanaji wa pembejeo bora na za gharama nafuu, pamoja na huduma za ugani zinazowafikia moja kwa moja shambani ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao yao.

Aidha, wakulima wameonesha imani kubwa kwa Serikali kutokana na hatua za kivitendo zinazochukuliwa, ikiwemo ushirikiano wa karibu na taasisi kama TFRA na TARI katika kupima udongo na kushauri matumizi sahihi ya mbolea. Wamesema matarajio yao ni kuona elimu hiyo ikiwafikia wakulima wengi zaidi ili kuboresha mavuno na kipato cha kaya.

Mkutano huo ulimalizika kwa matumaini mapya, huku wakulima wakiondoka wakiwa na ari ya kuongeza uzalishaji na kushirikiana na Serikali katika safari ya kukuza sekta ya kilimo. Hatua zilizopendekezwa na maagizo yaliyotolewa yametafsiriwa na wakulima kama suluhisho la changamoto nyingi, na uthibitisho kuwa kilimo kinaendelea kuwa injini ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.