KAMATI YA ADF YAJADILI MIPANGO YA UTEKELEZAJI KUKUZA SEKTA YA KILIMO
Kamati ya Ushauri ya Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (Agriculture Develeopment Fund -ADF) imefanya kikao kazi cha kwanza tangu kuundwa kwa Mfuko huo kwa dhumuni la kujadili mipango ya utekelezaji katika kukuza Sekta ya Kilimo nchini.
Mfuko huo umeanzishwa na Serikali kwa madhumuni ya kugharamia maeneo ya kimkakati yanayojitokeza kwa umuhimu ili kuchochea ukuaji na maendeleo ya kilimo; ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwekezaji katika miundombinu ya kilimo, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, zana za kilimo na ruzuku. Aidha, mfuko pia unalenga kuchochea uzalishaji wa Mazao unaozingatia viwango vya ubora na utengaji wa ulinzi wa maeneo ya kilimo.
Kikao kimefanyika tarehe 04 Septemba, 2025 katika Ukumbi wa mikutano Hazina, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Kamati wanaotokea Wizara ya Fedha; Wizara ya Kilimo; TAMISEMI; Wizara ya Viwanda na Biashara; Tume ya Mipango na Uwekezaji; Umoja wa Mabenki; na Vyama vya Ushirika.
Kikao kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Natu El-maamry Mwamba ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali; Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ambaye ni Katibu wa Kamati; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Athuman Kilundumya pamoja na Menejimenti za Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
Majadiliano ya Wajumbe yaliafiki mpango kazi na bajeti ya Mfuko ambayo itajikita katika ujenzi wa vituo vya ukusanyaji wa mazao ya horticulture, ununuzi na usimikaji wa mashine mbili za kuchakata zao la Mkonge, ujenzi wa maabara ya kuzalisha miche kwa njia ya chupa, ujenzi wa maabara ya afta ya mimea, ununuzi wa magari kwa ajili ya uhaulishaji wa teknolojia kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na ujenzi wa vituo jumuishi vya zana za kilimo.