Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MHE. PINDA AVUTIWA NA UBUNIFU WA VIJANA MAONESHO YA NANE NANE 2026

Imewekwa: 16 Sep, 2026
MHE. PINDA AVUTIWA NA UBUNIFU WA VIJANA MAONESHO YA NANE NANE 2026

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, ametembelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma, tarehe 6 Agosti 2026, ambapo amejionea mafanikio na ubunifu unaoendelea kuimarisha maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Mhe. Pinda ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho yanayowakutanisha wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kutoka ndani na nje ya nchi, yakionesha teknolojia, ubunifu na fursa zinazochochea ongezeko la uzalishaji na tija. Mhe Pinda alitembelea Banda maalum la vijana linalofahamika kama (Youth Innovation and Supermarket Pavilion) ambapo alijionea bunifu mbalimbali za vijana zinazolenga kutatua changamoto za sekta ya kilimo.

Bunifu hizo zinahusisha matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone) zenye Akili Unde (AI) katika kubaini magonjwa ya mazao mapema, sensa za udongo na mifumo ya umwagiliaji wa kisasa, mashine za kukaushia mazao kwa kutumia nishati ya jua na biogas, pamoja na uzalishaji wa mbolea za kikaboni kutoka mabaki ya mazao.

Mhe. Pinda pia ametembelea mabanda ya kampuni binafsi zinazojihusisha na uzalishaji wa mbegu bora, ambapo alijionea maendeleo ya teknolojia za uzalishaji wa mbegu zenye ubora na uwezo wa kuongeza tija kwa wakulima. Pia alipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi na wadau wa sekta ya kilimo katika kuendeleza uzalishaji wenye ushindani na unaokidhi mahitaji ya soko.

Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti, wawekezaji na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia bunifu na kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Maonesho ya Nanenane 2026 yanaongozwa na kaulimbiu: “Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza DIRA 2050”.