MWELI AIKARIBISHA MTW OJSC KUWEKEZA TANZANIA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amefanya ziara ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza matrekta kianchoitwa MTW OJSC (Minsk Tractor Works) kilichopo katika Jamhuri ya Belarus, tarehe 02 Juni 2026. Kiwanda hicho kinatengeneza matrekta na zana zake vikiwemo plau na haro. Trekta hizo zina ukubwa wa kuanzia hp 15 - 500 kulingana na mahitaji ya mkulima ndani na nje ya nchi ya Belarus.
Kampuni hiyo inatoa huduma mbalimbali ikiwemo matengenezo baada ya mauzo, mafunzo kwa maopareta na mafundi wa trekta na zana zake pamoja na kutoa ushauri wa kanuni bora za kilimo ili kuhakikisha matumizi sahihi ya matrekta na zana zake.
Kupitia mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha MTW OJSC , Katibu Mkuu Mweli ameikaribisha kampuni hiyo kuja kuwekeza Tanzania ikizingatiwa kuwa Tanzania imezungukwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Africa (AfCFTA) ambalo
ni soko muhimu la bidhaa zao.
Endapo uwekezaji huo utafanyika, utachochea ukuaji wa nchi kupitia ajira, kuongezeka kwa uzalishaji na mauzo nje ya nchi kwa mazao/chakula kitakachozalishwa kupitia matumizi ya zana za kilimo.
Katibu Mkuu Mweli amemwakilisha Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo katika ziara ya kikazi nchini Belarus ambapo amepokelewa na Mhe. Vitali Kulak, Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula wa Jamhuri ya Belarus.