Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

NFRA YATAKIWA KUIMARISHA HIFADHI YA CHAKULA; CPB YAASWA KUJIWEKEA MIKAKATI YENYE TIJA KATIKA KILIMO BIASHARA

Imewekwa: 10 Dec, 2025
NFRA YATAKIWA KUIMARISHA HIFADHI YA CHAKULA; CPB YAASWA KUJIWEKEA MIKAKATI YENYE TIJA KATIKA KILIMO BIASHARA

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA) imetakiwa kuimarisha hifadhi na usalama wa chakula nchini ili kufikia uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 700,000 ya nafaka.  Ameitaka pia NFRA kuendelea kupunguza madeni iliyonayo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha huduma kwa wakulima. 

Wito huo umetolewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) wakati wa Mkutano wake na NFRA na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) tarehe 8 Desemba 2025, jijini Dodoma.  

Waziri Chongolo pia ameitaka CPB kujiwekea mikakati yenye tija katika kilimo biashara badala ya kujiendesha kwa hasara.  “CPB ni taasisi ambayo inatakiwa kufikiria na kujiendesha kibiashara zaidi.  Tumieni vizuri miundombinu ya kibiashara iliyopo yaani viwanda, vihenge na maghala ili kuongeza toka katika biashara ya mazao ya kilimo,” amesisitiza Waziri Chongolo. 

Pamoja na mambo mengine, Taasisi hizo zimesisitizwa kushirikiana kwa pamoja katika kukuza Sekta ya Kilimo kutokana na uhitaji mkubwa wa mazao ya nafaka na mazao mengine.