Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SERIKALI KUIMARISHA MFUMO WA UZALISHAJI NA UDHIBITI WA MBEGU NCHINI

Imewekwa: 01 Jun, 2026
SERIKALI KUIMARISHA MFUMO WA UZALISHAJI NA UDHIBITI WA MBEGU NCHINI

Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa ubora wa mbegu kupitia taasisi za TOSCI na TARI kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na salama.

Amesema hayo Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo wakati akimwakilisha Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo katika Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu, tarehe 28 Mei 2026, jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa ongezeko la matumizi ya mbegu bora nchini limetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau pamoja na maboresho ya mifumo ya kidijitali ya usambazaji wa pembejeo za kilimo, hali inayosaidia kuongeza uwazi na ufanisi katika Sekta ya Kilimo.

Naibu Waziri Silinde pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza, katika kusaidia uzalishaji wa mbegu kupitia mashamba yao na hivyo kuongeza upatikanaji wake nchini.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Bw. Nyasebwa Chimagu, amesema kuwa mkutano huo unatoa nafasi kwa wadau mbalimbali kujadili maendeleo ya tasnia ya mbegu, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuboresha uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora nchini.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Mhe. Yustina Rahhi (Mb), ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa uzalishaji wa mbegu zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongezwa kwa elimu kwa wakulima ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo.