TANZANIA YAVUTIA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI KUTOKA POLAND
Tanzania imeendelea kufungua milango ya fursa za uwekezaji kimataifa huku Serikali ikiendelea kuvutia wawekezaji wenye tija katika Sekta za Uzalishaji kwa lengo la kuimarisha uchumi wa Taifa.
Hayo yametiliwa msisitizo wakati wa Mkutano wa Mawaziri kutoka sekta za uzalishaji nchini Tanzania na Bw. Marcin Kaleta, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Faspol Africa kutoka nchini Poland tarehe 26 Mei 2026, jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania ulihusisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru A. Kakurwa (Mb); Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David E. Silinde (Mb) aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo (Mb); Mhe. Dennis L. Londo (Mb); Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara; na Mhe. Dkt. Pius S. Chaya (Mb); Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji.
Majadiliano yamejikita pia kuhusu ushirikiano utakaochochea maendeleo ya Sekta za Kilimo; Mifugo na Uvuvi, hususan katika uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na upanuzi wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa na Sekta hizo ili kuleta tija, ajira, kuinua kipato zaidi kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Balozi John Ulanga; mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara ya Kilimo.