UZALISHAJI WA ALIZETI IKUNGI, ITIGI, IRAMBA NA MKALAMA MKOA WA SINGIDA
Wakulima wa zao la Alizeti katika Halmashauri za Wilaya za Ikungi, Itigi, Iramba na Mkalama mkoani Singida wameendelea kunufaika na elimu ya kanuni bora za kilimo cha Alizeti kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa na Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania (TAISP) unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo.
Zoezi la ufuatiliaji wa mashamba darasa ya Alizeti limefanyika tarehe 12-13 Mei 2026 mkoani Singida katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Singida Manispaa kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanazingatia kanuni bora za kilimo na kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti.
Kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji, jumla ya wakulima 807 wamenufaika na mafunzo hayo katika halmashauri za Itigi (278), Ikungi (192), Iramba (157) na Mkalama (180), kupitia mashamba darasa ya alizeti yaliyoanzishwa na TAISP.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye pia ni Afisa Kiungo wa TAISP, Bw. Bruno John Magazi, amesema Wizara ya Kilimo imewezesha upatikanaji wa pembejeo ikiwemo mbegu bora na mbolea za kupandia na kukuzia, hatua iliyowezesha wakulima kujifunza kwa vitendo kilimo cha kisasa chenye tija.
Kwa upande wa Afisa Kilimo wa Kata ya Dung’unyi (Ikungi), Bi. Ester Simon Bayda; Afisa Mazao wa Itigi, Bw. Christopher Wilboard Ghumpi; na Afisa Kilimo wa Kata ya Tumuli (Mkalama), Bi. Veronica Josia Bathlomeo, wameiomba Serikali kuendelea kuwezesha upatikanaji wa mbegu kwa bei nafuu, kuendeleza elimu ya kilimo na kuongeza idadi ya mashamba darasa ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Kwa pamoja, wakulima akiwemo Bi. Pili Isingo Siuhi (Ikungi), Bi. Janet Emmanuel Kitinka (Itigi), pamoja na wakulima wa Iramba na Mkalama akiwemo Bw. Miraji Athuman Mtitu na Bi. Rehema Kyula Nonti, wamesema mashamba darasa yamewasaidia kuongeza uelewa wa kilimo bora cha Alizeti na kuwapa matumaini ya kupata mavuno mengi kupitia mbegu bora za AGUARA 6 na HYSUN 33.
Naye, Afisa Kiungo wa TAISP katika Halmashauri ya Iramba, Bi. Emakulatha Peter Sulle, ameeleza kuwa mashamba darasa yamekuwa yakiwajengea uwezo wa kulima kisasa na kuongeza kipato cha kaya.