VIJANA KUNUFAIKA NA AJIRA 6000 ZA MRADI WA BBT
Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Kilimo, Unenepeshaji wa Mbuzi na Kilimo cha Malisho unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi umejipanga kuhakikisha unatoa ajira 6000 kwa wanawake na vijana nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano cha utekelezwaji wake.
Meneja Mradi wa BBT Upande wa Jinsia na Ujumuishaji wa Kijamii, Bi. Neema Urassa katika wasilisho lake alilolitoa tarehe 01 Juni 2026 mkoani Morogoro kwenye Warsha ya Upitiaji, Uhakiki wa Uwasilishaji wa Ripoti ya awali ya Jinsia na Ujumuishaji wa Kijamii katika Programu BBT, amesema kuwa mradi huo utakuwa na fursa kubwa kibiashara kwa Wanawake na Vijana kupitia shughuli za unenepeshaji wa mbuzi na kondoo pamoja na fursa za kilimo cha malisho ya mifugo.
"Wanufaika watajifunza vitu mbalimbali kwa vitendo katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya mifugo, hususan mbuzi na kondoo na kilimo cha malisho ya mifugo, ili baadae wawe na uwezo wa kuingia kwenye biashara za unenepeshaji wa mifugo kwa lengo la kujiongezea kipato pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa," amesema Bi. Urassa.