WADAU WA MAENDELEO WAPONGEZA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA MIFUMO HIMILIVU YA CHAKULA
Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (International Fund for Agricultural Development - IFAD) na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan - JICA) umeendelea na ziara yake nchini kwa kukutana na majadiliano na timu ya wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) ikiwa ni sehemu ya kukagua utekelezaji wa programu hiyo (implementation support mission).
Mkutano huo umefanyika tarehe 01-02 Oktoba 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Kilimo, jijini Dodoma. Awali, ujumbe huo ulifanya ukaguzi katika kituo cha utafiti wa kilimo cha TARI- Tengeru; TARI- Seliani na shamba la mbegu za kilimo la Ngaramtoni la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), jijini Arusha tarehe 29 Septemba 2025; na skimu ya umwagiliaji iliyopo Mapama katika Wilaya ya Meru chini ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) tarehe 30 Septemba 2025.
Katika majadiliano ya mapitio ya taarifa za utekelezaji wa miaka miwili wa miradi mbalimbali chini ya programu ya TPSRF na mpango kazi wa mwaka 2025/2026 wa TFSRP, ujumbe huo uliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri inayoendelea ya kuleta mapinduzi katika Sekta ya Kilimo hususan kwa wakulima wadogo ili wapate tija katika mavuno yao.
Ujumbe uliihakikishia Wizara ya Kilimo ushirikiano katika maeneo mbalimbali yaliyokubalika yakiwemo uchimbaji wa visima kwa wakulima wadogo, uboreshwaji miundombinu ya tafiti za kilimo na kidijitali ili huduma kwa wakulima ziendelee kuwafikia, mafunzo kwa Maafisa Ugani na vitendea kazi, na mengine.
Aidha, majadiliano pia yalihusisha kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi ambapo Bw. Timotheo Semuguruka, Mratibu wa programu ya TFSRP alieleza kuwa Wizara ya Kilimo imeanza kushirikisha Vyama vya Ushirika kwa lengo la kuhakikisha mahitaji ya wakulima yanafikiwa kwa wakati kupitia ushirikishwaji wa Sekta Binafsi.