WAKULIMA 94 MISUNGWI WAPOKEA VIFAA VYA KISASA VYA UMWAGILIAJI
Wizara ya Kilimo kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) imekabidhi vifaa vya kisasa vya umwagiliaji kwa vikundi vitatu vyenye jumla ya wakulima 94 wa mazao ya bustani, matunda na mazao mengine ya chakula katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoa wa Mwanza.
Mgao huo ni sehemu ya usambazaji wa vifaa vya umwagiliaji jozi 200 katika mikoa saba kwa awamu ya kwanza ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Ruvuma, Tanga na Simiyu vyenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 3.5, ili kuongeza tija katika kilimo, kipato cha wakulima na kupunguza utegemezi wa mvua.
Akizungumza tarehe 10 Novemba 2025 wakati wa makabidhiano hayo, Mhandisi Makubi Abel kutoka Wizara ya Kilimo amesema wakulima wanapaswa kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi ili kuongeza uzalishaji, akibainisha kuwa mpango huo unalenga kusaidia wakulima wadogo kugeuza kilimo kuwa shughuli endelevu na yenye faida inayomfanya mkulima aweze kulima mwaka mzima bila kutegemea misimu pekee ya mvua.
Kwa upande wake, Dkt. Chrispine Shami, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ameeleza kuwa kabla ya usambazaji wa vifaa hivyo, wakulima wengi walikosa vifaa vya kisasa vya umwagiliaji, jambo lililokuwa likipunguza uzalishaji na kuathiri ubora wa mazao. Ameeleza vifaa hivyo vitasaidia kuongeza tija na kuvutia vijana wengi zaidi katika Sekta ya Kilimo.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Addo Missama amesema utoaji wa vifaa hivyo ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa wakulima na maendeleo ya Wilaya, huku akisisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza kipato chao.
Baadhi ya wanufaika wa programu hiyo ambao ni wakulima wamesema vifaa hivyo vya kisasa vitawawezesha kumwagilia eneo kubwa la mashamba yao kwa haraka na kwa muda mfupi itakayopelekea kuongeza tija na uzalishaji.