Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA KUNUFAIKA NA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA INDONESIA

Imewekwa: 11 May, 2026
WAKULIMA KUNUFAIKA NA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA INDONESIA

Wakulima nchini wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa pembejeo bora; uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa zao la chikichi; biashara pamoja na masoko ya mazao mbalimbali ya kilimo kimataifa.

Hayo yamebainishwa kupitia Kikao cha Nne cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo baina ya Tanzania na Indonesia (4th Joint Agriculture Cooperation Committee - JACC) kilichofanyika tarehe 5-7 Mei, 2026 jijini Dodoma, kikilenga kukuza Sekta ya Kilimo na uchumi wa pande zote mbili. 

kikao hicho pamoja na mambo mengine kimejadili umarishwaji wa ushirikiano katika uzalishaji wa mbolea, ili kukidhi mahitaji ya mbolea yanayokadiriwa kufikia metric tonnes 1,200,000 kwa mwaka 2026/2027, na kupunguza uingizwaji wa mbolea kutoka nje ya nchi.

Aidha, kikao hicho pia kimejadili upatikanaji wa mafuta kwa kuongeza uzalishaji wa chikichi; kuimarisha utafiti na teknolojia katika zao hilo; kuongeza uzalishaji wa miche bora pamoja na  kubadilishana teknolojia baina ya Tanzania na Indonesia, ushirikiano ambao unaendelea hadi hivi sasa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), na Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Mkindo kilichopo mkoani Morogoro.

Kikao hicho ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia katika kilimo ambapo, kikao cha tatu cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo cha November, 2014 kilijikita katika kukuza ushirikiano; maendeleo ya tafiti; zana za kilimo pamoja na upatikanaji wa masoko.