WAZIRI CHONGOLO AWASILISHA HOTUBA YA WIZARA YA KILIMO
Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Godfrey Chongolo (Mb), akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2026/2027 tarehe 28 April 2026 Bungeni jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, Mhe. Chongolo amesema Sekta ya kilimo imeendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, upatikanaji wa ajira, malighafi za viwandani na kuchangia katika Pato la Taifa (GDP). “Katika mwaka 2025, Sekta ya Kilimo imekua kwa asilimia 4.0. Aidha, imechangia asilimia 24.6 katika Pato la Taifa.”
Vilevile, ameeleza kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2024/2025 ulifikia tani milioni 23.78 ikilinganishwa na tani milioni 22.8 katika msimu wa kilimo wa 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.3 na kufanya utoshelevu wa chakula nchini kufikia asilimia 130.
Pia ameeleza kuwa Wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kuanzisha Wakala ya Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo (NAESA), ambao inatarajiwa kuanza rasmi mwaka mpya ujao wa fedha (Julai 2026). Wakala huo utawezesha kuongeza ufanisi wa huduma za ugani, kuratibu na kusimamia shughuli za ugani na kuhaulisha teknolojia kutoka kwa watafiti na wadau wengine kwenda kwa maafisa ugani na wakulima.