Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI CHONGOLO: MPANGO NA BAJETI YA WIZARA 2026/2027 UMEBEBA MAONO MAPANA YA SERIKALI

Imewekwa: 29 Apr, 2026
WAZIRI CHONGOLO: MPANGO NA BAJETI YA WIZARA 2026/2027 UMEBEBA MAONO MAPANA YA SERIKALI

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Godfrey Chongolo (Mb), ameeleza kuwa mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo katika mwaka 2026/2027, umebeba maono mapana ya Serikali kupitia kilimo ambayo ni msingi na dira itakayoiwezesha Tanzania kufikia hadhi ya nchi ya kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka 2050 kupitia utekelezaji wa vipaumbele sita (6)

Mhe. Chongolo amesema vipaumbele hivyo ni: kuongeza tija na uzalishaji; kuchangia kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo; kuimarisha usalama wa chakula na lishe; kuimarisha upatikanaji wa mitaji, masoko na mauzo ya mazao nje ya nchi.

Vilevile ameeleza kuwa Wizara itaendelea kuimarisha maendeleo ya ushirika pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika uendelezaji wa sekta ya kilimo.

Aidha Mhe. Chongolo amesema katika kuimarisha mahusiano na jamii (Corporate Social Responsibility – CSR), Wizara kupitia taasisi zake itatekeleza miradi itakayolenga kuimarisha uzalishaji wa mazao kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha na kutoa motisha kwa jamii husika kushiriki katika shughuli za kilimo hususan vijana na wanawake.