Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI MKUU AZINDUA SOKO LA MAZAO KIBAKWE

Imewekwa: 11 May, 2026
WAZIRI MKUU AZINDUA SOKO LA MAZAO KIBAKWE

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amezindua rasmi Soko la mazao ya Kilimo Kibakwe lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa tarehe 9 Mei 2026, mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya kilimo na biashara ya mazao nchini.

Akizungumza na wananchi baada ya uzinduzi wa soko hilo, Mhe. Dkt. Mwigulu amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi wa matokeo kwa kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania

“Mheshimiwa Dkt. Samia ni  mtendaji ambaye akisema jambo, anatekeleza. Na haya yanadhihirishwa kwa kazi kubwa ambayo imefanyika,” ameeleza Dkt. Mwigulu.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo,Mhandisi Athuman Kilundumya amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi ya kimkakati katika sekta ya kilimo kwa kuboresha miundombinu ya masoko, uhifadhi na usafirishaji wa mazao.

Ameeleza kuwa mradi wa Soko la Kibakwe ni miongoni mwa miradi minne inayotekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Tabora chini ya Programu ya Tanzania Food Systems Resilience Program (TFSRP), kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 3.6.

Kuhusu Soko la Kibakwe, amesema mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 603 na umefikia asilimia 98 ya utekelezaji unaoruhusu kuanza kutumika huku kazi zilizobakia zikiwa ni hatua za mwisho za umaliziaji.

Mha. Kilundumya ameeleza kuwa soko hilo linatarajiwa kuhudumia wafanyabiashara na wakulima kati ya 300 hadi 350 kwa wakati mmoja, na litasaidia kuongeza upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao mbalimbali ikiwemo alizeti, karanga, mtama na mbogamboga.

Mradi huo utaongeza ajira kwa vijana na wanawake, kuongeza kipato kwa wakulima pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia shughuli za biashara.

Wananchi wa eneo la Kibakwe wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya masoko, wakisema hatua hiyo itarahisisha biashara ya mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo.