Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chakula (NFRA)
Histori ya kuanzishwa kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inarudi nyuma kwenye tatizo la ukame lililojitokeza miaka ya 1973 - 1975 wakati Tanzania ilipopata athari kubwa ya upungufu wa chakula hivyo kushindwa kumudu mahitaji ya ndani ya chakula na kulazimika kuagiza chakula kutoka nje ya nchi. Hali hiyo ilisababisha Serikali kuanzisha Hifadhi ya Chakula ya Taifa (Strategic Grain Reserve - SGR) mwaka 1976 ikiwa ni mbinu ya kuiwezesha kuepuka au kupunguza makali ya upungufu wa chakula nchini. Kutoka kipindi hicho SGR ilifanyiwa mabadiliko mbalimbali ya kimuundo na uwajibikaji. NFRA iliundwa kuchukua majukumu wa SGR ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula - National Food Reserve Agency (NFRA) ni Taasisiya Umma iliyo chini ya Wizara ya Kilimo. Wakala ulianzishwa kwa Sheria ya Wakala za Serikali Sura 245 (Na. 30/1997), kama ilivyorekebishwa na Sheria namba 13 ya mwaka 2009, ikisomwa pamoja na Hati Rasmi iliyoanzisha NFRA mwaka 2008 kupitia Tangazo la Serikali Na. 81 la tarehe 13 Juni, 2008 na kuhuishwa na Tangazo la Serikali Na. 120 la mwaka 2016.
Dira “Kuwa Wakala wa kuaminika wenye uwezo wa kukabiliana na upungufu wa chakula kwa wakati”.
Dhima “Kuhakikisha upatikanaji wa akiba ya chakula cha kimkakati wakati wa upungufu wa chakula kwa kununua, kuhifadhi, kuzungusha na kutafuta masoko ya chakula kwa ufanisi na kwa manufaa ya jamii.”
Maadili ya Msingi
- Ufanisi
- Kuaminika
- Uweledi
- Uadilifu
- Kumjali mteja
- Uwazi
- Uwajibikaji
- Ubunifu
- Kufanya kazi kwa pamoja
Majukumu
Ili kufikia dira na dhima, Wakala unatekeleza majukumu yafuatayo:-
- Kuhifadhi akiba ya chakula toshelevu kwa mahitaji ya nchi;
- Kununua, kuhifadhi na kutoa akiba ya chakula ili kukabiliana na majanga;
- Kuzungusha na kutafuta masoko ya chakula ili kupunguza mfumuko wa bei na kuingiza mapato;na
- Kutoa huduma mbalimbali za uhifadhi ili kuongeza mapato.
Katika kutekeleza majukumu hayo, Wakala huweza kutumia vyanzo vifuatavyo vya Mapato:
- Ruzuku kutoka Serikalini;
- Mauzo ya akiba ya chakula;
- Fedha zinazopatikana kutokana na huduma zinazotolewa na Wakala;
- Mikopo kutoka taasisi za fedha;
- Misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo.