Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

ASA YATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU YA MPUNGA SARO 5 (TXD 306)

Imewekwa: 04 Aug, 2026
ASA YATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU YA MPUNGA SARO 5 (TXD 306)

Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) umetakiwa kuongeza uzalishaji wa mbegu ya Mpunga aina ya Saro 5 (TXD 306) kutokana na uwezo wake wa kustahimili magonjwa, ukame na kustawi katika mazingira mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe,  alipotembelea banda la ASA katika Maonesho ya Kimataifa Saba Saba, jijini Dar es Salaam tarehe 03 Julai 2026, na kuzungumza na wataalamu wa Wakala huo.

Prof. Msoffe amesema kuwa mbegu hiyo ni bora na yenye tija kwa wakulima kwani huzalisha mavuno mengi, hivyo kuwanufaisha kiuchumi. Ameitaka ASA kuendelea kuizalisha kwa wingi na kuhakikisha inasambazwa nchini. 

Aidha, katika kuimarisha nafasi ya ASA, Naibu Katibu Mkuu Prof. Msoffe amesisitiza umuhimu wa Wakala kutoa elimu, mafunzo na kufanya kampeni za uhamasishaji ili wakulima wengi waweze kufahamu ubora wa mbegu hizo na kuzinunua.  Hatua hiyo itachangia katika kukuza kilimo chenye tija, kuboresha maisha ya familia za wakulima na kuendeleza ustawi wa Taifa kwa ujumla.