BARAZA LA HORTI LOGISTICA AFRICA LAZINDULIWA RASMI DAR ES SALAAM
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, amezindua rasmi Baraza la Horti Logistica Africa tarehe 12 Novemba, 2025 katika Mkutano Mkuu wa Kilimo na Biashara wa Mazao ya Mboga Mboga na Matunda uliofanyika katika Hotel ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.
Baraza hilo litafanyika mwezi Novemba kila mwaka nchini na kuwakutanisha wadau wa Tasnia ya Horticulture Duniani hapa barani Afrika, kushuhudia uzalishaji na uchumi wa tasnia ya mazao ya bustani, likiwa ni jukwaa la kujifunza kuhusu changamoto, mafanikio na fursa ya tasnia hiyo kuanzia shambani hadi sokoni.
Dkt. Yonazi amemwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka kama mgeni rasmi ambapo ameipongeza Wizara ya Kilimo pamoja na Asasi Kilele ya Sekta Binafsi inayoendeleza na kukuza Sekta ya Horticulture nchini (TAHA) kwa utekelezaji wa dira na mwelekeo wa Sekta ya Kilimo katika mifumo, masoko na ujuzi, akisema Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuboresha miundombinu ya uhifadhi, usafirishaji pamoja na masoko, ili kukuza horticulture inayotoa ajira kwa vijana na wanawake, katika kukuza na kujenga uchumi shirikishi nchini.
Hadi kufikia mwaka 2024, TAHA imerekodi mapato ya Dola za Marekani Milioni 569 ya mauzo ya mazao ya horticulture nje ya nchi ikiwa ni ongezeko kutoka Dola za Marekani Milioni 290.7 zilizorekodiwa kwa mwaka 2020 ikiwa ni mafanikio makubwa kwa horticulture nchini.
Amehitimisha kwa kuitaka TAHA kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuwezesha Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Horticulture kufanyika kila tarehe 1 Agosti ya mwaka nchini katika Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane, ili kuwafikia wakulima katika ngazi zote nchini na kutoa fursa kwa wadau kujadili na kutatua changamoto zozote za kuimarisha Tasnia ya Horticulture horticulture nchini.