BARAZA LA KUMSHAURI RAIS LAKUTANA NA WIZARA KUJADILI UTEKELEZAJI NA USHIRIKIANO
Baraza la Kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusu Utekelezaji wa Masuala ya Kilimo na Chakula likiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda, limekutana kwa mazungumzo na Viongozi wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi tarehe 24 Machi 2026, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza, Mhe. Pinda amesema kuwa aliona ni busara timu yake ikakutana na Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo na Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi ili kutoa taarifa ya utekelezaji wao tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo na kuimarisha ushirikiano.
Mhe. Pinda amesema kupitia ushirikiano na Wizara hizo mbili, Baraza limepata nafasi ya kukutana na Wadau zaidi ya 1570 katika Kanda mbalimbali wakiwemo Sekta Binafsi; pia na kutembelea shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi zinazofanywa na vijana na wanawake.
Naye Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo amesema kuwa kilimo kimekuwa moja ya vipaumbele vya Serikali ambapo uwekezaji wake umechangia kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Shilingi Bilioni 294 hadi zaidi ya Shilingi Trilioni 1.2 katika kipindi cha miaka mitatu.
“Tija imekuwa msingi wa uzalishaji, hususan katika eneo la umwagiliaji kwa asilimia zaidi ya 60 ya bajeti imeelekezwa kwenye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ambapo zaidi ya miradi 740 ya umwagiliaji imepangwa kutekelezwa. Pia masoko 14 yamepatikana nje ya nchi kwa mfano viazi na matunda ambapo yanahitaji uwekezaji kwenye usafirishaji, uhifadhi na teknolojia za ukaushaji,” amesema Waziri Chongolo.
Naye Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi amesema kuwa Sekta hizi mbili zimedhamiria kushirikiana kwa umoja katika kusimamia utekelezaji maono na matamanio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu la utu kwa Watanzania ili kuhakikisha kuna utoshelevu na usalama wa chakula nchini.
Msingi wa kuanzisha Baraza hilo ni matokeo ya Mkutano wa utoshelevu na ustahimilivu ulifanyika mwaka 2023 Dakar, nchini Senegal ambapo Wakuu wa Nchi za Afrika waliazimia kuwa na Baraza la kushauri mageuzi katika Sekta ya Kilimo; ikiwemo kushirikisha Sekta Binafsi; kushirikisha vijana na Wanawake katika mnyororo mzima wa uzalishaji; matumizi ya ardhi katika kilimo na malisho ya mifugo na uvuvi.