BASHE: KILIMO NI SAYANSI NA NI UCHUMI

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema safari ya mabadiliko katika Sekta ya Kilimo siyo ya kubahatisha ‘betting’ bali ni sayansi na uchumi.
Ameeleza zaidi kuwa hakuna njia za mkato kwenye shughuli za kilimo, kwa kuwa bei ya zao inaamuriwa kwa sayansi na hesabu siyo kukaa mezani kucheza kamari ‘bet’.
Waziri Bashe amesema hayo wakati wa Mkutano wa hadhara wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya stendi ya zamani, wilaya ya Bariadi, Mkoani Simiyu tarehe 18 Juni 2025.
“Mhe. Rais, tunaenda kujenga kongani ya viwanda (industrial park) ndani ya Mkoa wa Simiyu ambayo litakuwa na Viwanda vidogo vya uchakataji wa marobota na Serikali imetoa Shiling Bilioni 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kongania hiyo ambapo Serikali ita gharama umeme, maji na maghala. Hivyo, wawekezaji watafunga mashine tu za uchakataji,” amesema Waziri Bashe.
Aidha, Waziri Bashe amesema kuwa zao la Korosho limenufaisha wakulima kutokana na ruzuku hivyo ili kuongeza tija ya uzalishaji wa Pamba, Serikali imetoa ruzuku ya mbegu na viuatilifu bure kwa wakulima.
Pia Serikali imechukua hatua ya kusambaza Vinyunyizi vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 3, matrekta 205 ambapo wakulima watachangia Shilingi 35,000 kama tozo ya kulimiwa kwa ekari.
“Msiende kuangusha bei kwa wakulima wa Pamba kwa kuwatishia bei kama miaka ya huko nyuma iliyoshusha bei ya zao hilo hadi shilingi 500. Kumbukeni bei ya Pamba haiamuriwi katika mikutano ya hadhara bali ni sayansi ya hesabu hutumika kulingana na soko la Dunia, Niwahakikishie Serikali itawalinda wakulima,” amesema Waziri Bashe.
Hatua hiyo ni dhamira ya Serikali kuinua zao la Pamba ili kilo 1000 iweze kupatikana katika ekari moja; ikiwa ni pamoja na kujenga pia maghala yapatao 300 ya kuhifadhia Pamba na mazao ya kilimo kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe pia amewatoa hofu wakulima wa Mbaazi kuwa mnada wa kwanza utafanyika tarehe 20 Juni 2025 siku ya ijumaa katika wilaya ya Bariadi na kuwataka magagaranja wafuate utararibu; kwa kuwa bei itajulikana siku hiyo.