BASHE: SERIKALI KUJA NA MIKAKATI KUPUNGUZA GHARAMA ZA MBOLEA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amekutana na wazalishaji wa mbolea yabisi na visaidizi vya mbolea nchini ili kujadili na kuja na mpango wa namna ya kuongeza uzalishaji na matumizi ya mbolea na visaidizi vya mbolea zinazozalishwa nchini.
Mkutano huo umefanyika tarehe 12 Juni 2025 ambapo pia walishiriki Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo na Bw. Joel Laurent, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Waziri Bashe alisema kuwa lengo la mpango huu,pamoja na mambo mengine ni kuongeza uzalisha wa mbolea na visaidizi vya mbolea nchini na kuongeza matumizi ya mbolea za ndani ili kuondokana na hali ilivyo sasa ambapo takribani tani miloni 1.2 zinaagiwa kutoka nje ya nchi.
Aidha, Waziri Bashe amesema mpango huu pia unalenga kuyafikia maeneo ambayo matumizi ya mbolea na visaidizi vya mbolea yapo chini au hayapo kabisa.
Aliongeza kuwa mbolea hizo zitazalishwa kwa kuzingatia afya ya udongo na mahitaji ya mimea ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini.
Kuhusu matumizi ya visaidizi vya mbolea nchini kuwa bado yapo chini, Waziri Bashe amesema kuwa mpango huu unatarajiwa kuongeza matumizi ya visaidizi vya mbolea ambavyo hurekebisha hali ya udongo wenye tindikali na kuwezesha mmea kufyonza kwa ufanisi virutubisho kutoka kwenye udongo.
Kadhali, Waziri Bashe alisema kupitia mpango huu, Serikali inatarajia kununua kiasi cha tani 200,000 za mbolea yabisi zinazozalishwa nchini (Compounded fertilizers) na tani 50,000 za visaidizi vya mbolea na kuzisambaza kwa wakulima kupitia utaratibu maalum utakaowekwa.