BASHE: SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI KWA WAUZAJI WA MBEGU FEKI NCHINI

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema Serikali iko mbioni kutunga Sheria itakayowabana wauzaji wa mbegu, viuatilifu na mbolea feki ili waweze kuhukumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi kuanzia msimu ujao wa kilimo.
Waziri Bashe amesema hayo akiwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu tarehe 15 Mei 2025 uliofanyika katika Ukumbi wa Midland Hotel, jijini Dodoma.
“Sheria iliyopo sasa haina meno ya kuwabana wauzaji wanaobainika kuuza mbegu feki kwa kuwa faini wanazotozwa ni ndogo kuliko hasara wanayoisababisha katika jamii”, amesema Waziri Bashe.
Ameongeza kuwa mtu anayewauzia wakulima mbegu feki anatakiwa kuhukumiwa lakini sheria iliyopo sasa inawatoza wauzaji hao faini kati ya Shilingi 500,000/= hadi shilingi 1,000,000/= ambayo hailingani na makosa waliyoyafanya.
Aidha, Waziri Bashe ametoa rai kwa wauzaji wa mbegu na wasambazaji wote wa Mbegu nchini kuwa waaminifu na kuhakikisha wanauza na kusambaza mbegu bora na halali ambazo zina nembo ya Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) ili zitumike kwa kuleta uzalishaji wenye tija kwa wakulima ili kuendana na azma ya Serikali katika Agenda 10/30.