BASHE: TOSCI SHIRIKIANENI NA TAKUKURU KUDHIBITI TATIZO LA MBEGU FEKI
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe ameiagiza Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kudhibiti uuzaji na usambazaji wa mbegu feki nchini.
Ametoa maagizo hayo tarehe 22 Agosti 2025 jijini Dodoma, wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Amesema kuwa tatizo la mbegu feki ni changamoto kubwa kwa wakulima na maendeleo ya kilimo nchini, hivyo ni lazima TOSCI na TAKUKURU waimarishe ushirikiano wao ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinaathiri maendeleo ya kilimo kwa wakulima nchini.
Aidha, Waziri Bashe ameigiza Bodi ya TOSCI kuhakikisha inakaa kwa pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ili kuongeza tija na uzalishaji wa Tasnia ya Mbegu nchini.
Katika hafla hiyo, Waziri Bashe ameambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya pamoja na wataalam kutoka Menejimenti ya Wizara ya Kilimo.
Ifahamike kuwa mahitaji ya mbegu bora kwa mwaka ni tani 127,650 katika mwaka 2025/2026, ambapo uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 63,526.54 hadi tani 90,000; huku upatikanaji wa mbegu bora nchini unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 79,700.62 hadi tani 105,000.