BBT CHINANGALI YAPONGEZWA
Mwenyekiti wa Baraza la Kumshauri Rais kuhusu masuala ya Chakula na Kilimo na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda amefurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika Shamba la pamoja la BBT Chinangali, na kuwataka wanufaika wa Programu hiyo kuongeza bidii ya uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kuongeza tija na kipato.
Mhe. Pinda amesema hayo alipotembelea shamba hilo lililopo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 16 Desemba 2025 na kueleza kuwa kumekuwa na matukio mbalimbali yanoyuhusisha matumizi yasiyo sahihi ya miundombinu ya umwagiliaji ambayo hutumika kunywesha mifugo na kuleta uharibifu, hivyo ni vyema kuhakikisha miundombinu inayojengwa inazingatia pia matumizi ya mifugo.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya amesema kuwa Serikali inaanzisha mashamba ya malisho ya mifugo wilayani Kongwa katika kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) kuhusu uanzishwaji wa mashamba hayo.
Aidha, Mratibu wa Programu hiyo Bw. Clepin Josephat amesema Programu hiyo inatekelezwa kwa muda wa miaka 8 ikilenga kuongeza tija na uzalishaji, ajira zenye staha, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza ustawi wa jamii, ikilenga kuwafikia wanufaika Milioni kumi (10,000,000) pamoja na vijiji 12,000 nchini.
Amehitimisha kwa kusema programu hiyo imejikita katika maeneo (5) ya kimkakati ikiwemo uchimbaji wa visima, huduma za ugani, mkopo wenye riba nafuu kwa vijana pamoja na uongezaji thamani.