Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA (TADB) MDHAMINI MKUU MAONESHO YA NANE NANE 2025

Imewekwa: 01 Aug, 2025
BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA (TADB) MDHAMINI MKUU MAONESHO YA NANE NANE 2025

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amepongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuwa Wadhamini Wakuu wa Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane 2025 kwa mchango wa shilingi milioni 400. 

Hafla ya kupokea hundi hiyo imefanyika tarehe 31 Julai 2025 katika Viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.

Katibu Mkuu Mweli amesema Benki ya TADB imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za maendeleo ya wakulima na mchango wao ni ishara kubwa kwa kuwa Benki hiyo pia inaadhimisha Miaka 10 toka kuanzishwa kwake hapa nchini.

Ameongeza zaidi kuwa Maonesho ya Nane Nane 2025 yameboreshwa zaidi na ni kitivo cha elimu kwa wakulima na wafanyabiashara katika mnyororo wa thamani wa kilimo.  Fursa za elimu na huduma za kifedha zitatolewa na Benki ya TADB ambayo imekuwa ikirahisisha upatikanaji wa mitaji ya kilimo kupitia mikopo na ruzuku kwa wakulima.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TADB, Bw. Frank Nyabundege amesema Benki inatambua umuhimu wa Maonesho hususan kwa wakulima, wafugaji na wavuvi na ndiyo msingi wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza Sekta ya Kilimo inayoajiri 75% ya Watanzania hapa nchini.