BETI YA WIMBO WA TAIFA YAWA CHACHU YA KUIMARISHA USHIRIKIANO
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amesema kuwa beti ya kwanza ya wimbo wa Taifa “Mungu Ibariki Afrika….hekima umoja na amani….ibariki Afrika na watu wake….”, ni kielelezo kinachochochea mshikamano na ushirikiano wa Mataifa ya Afrika katika kuimarisha uzalishaji wa chakula na biashara ya mazao ya kilimo.
Amesema hayo tarehe 13 Machi 2026 wakati wa mazungumzo yake na Bw. Tony Bandio Munongo, Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika masuala ya Uchumi na Uwekezaji.
“Ningependa kuona nchi zetu zinaimarisha na kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara katika nyanja mbalimbali za kiuchumi. Inasikitisha kuona nchi kama India, Amerika ya Kusini likiwemo Bara la Ulaya zinakuwa wadau wakubwa wa kulisha baadhi ya nchi za Afrika kama Kongo - DRC; wakati Tanzania ina utoshelevu wa chakula cha ziada kufanya biashara,” amesema Waziri Chongolo.
Waziri Chongolo amesema kuwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kukuza Sekta ya Kilimo kwa kuongeza uzalishaji; huku akitolea mfano wa mafanikio katika usalama wa chakula ambapo Tanzania imefikia utoshelezi wa chakula kwa asilimia 128 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 114 mwaka 2021.
Aidha, Waziri Chongolo ameeleza kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ina uhifadhi wa ziada wa chakula kwa zaidi ya tani laki nne za mahindi ambapo NFRA iko tayari kuiuzia Kongo - DRC endapo itahitaji kuuziwa kama nafaka au unga wa mahindi.