Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO AIPONGEZA TARI KWA MIAKA 10 MAGEUZI YA TAFITI, AKABIDHI VITENDEA KAZI

Imewekwa: 24 Apr, 2026
CHONGOLO AIPONGEZA TARI KWA MIAKA 10 MAGEUZI YA TAFITI, AKABIDHI VITENDEA KAZI

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imepongezwa kwa kazi nzuri ya kuleta mageuzi katika tafiti za mbegu nchini na kukabidhiwa pikipiki 71 zitakazoleta tija zaidi kwa watafiti.

Amesema hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) tarehe 23 Aprili 2026 jijini Dodoma na kuongeza kuwa pikipiki hizo zitaleta mapinduzi makubwa katika utendaji kazi wa watumishi wa TARI katika vituo vyote vya utafiti na mashamba ya majaribio.
 
Hafla hizo zimeshirikisha Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb); Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya; Menejimenti ya TARI iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Thomas Bwana; Mkurugenzi Dkt. Sophia Kashenge; Watafiti kutoka Vituo mbalimbali vya TARI nchini. 
 
Kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Waziri Chongolo ameipongeza TARI kwa kuja na Wazo nzuri la kuanzisha “Marathon ya TARI” na kuwataka waipange rasmi katika siku maalum kwenye wiki ya Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane 2026 ambapo Wadau wengi wa Kilimo watapata fursa ya kushiriki, akiwemo mwenyewe. 

Maadhimisho haya yatafanyika rasmi tarehe 24–26 Juni 2026, jijini Dodoma, yakibebwa na kaulimbiu isemayo: “A Decade of Impact: Shaping the Future of Agriculture in Tanzania,” ambayo inaakisi mafanikio ya TARI na mwelekeo wake wa baadaye.  Pia yatatumika kuwasilisha dira ya kimkakati ya mwaka 2026–2035 inayolenga kuimarisha ubunifu, kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza kilimo jumuishi na endelevu.

Tangu kuanzishwa kwake, TARI imekuwa nguzo muhimu ya utafiti wa kilimo kupitia kuendeleza teknolojia bunifu na suluhisho za kisayansi zilizochangia kuongeza usalama wa chakula, kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo.