Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO AITAKA TPHPA KUJA NA DRONES ZA KUPULIZIA KOROSHO

Imewekwa: 04 Aug, 2026
CHONGOLO AITAKA TPHPA KUJA NA DRONES ZA KUPULIZIA KOROSHO

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imetakiwa kuja na teknolojia ya ndege nyuki (drones) kwa ajili ya upuliziaji wa viuatilifu kwenye zao la Korosho katika msimu huu wa kilimo. 

Hayo yamehimizwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi Makao Makuu ya TPHPA jijini Arusha tarehe 3 Julai 2026 ambapo amelakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru. 

Amesema majaribio hayo yatasaidia kubaini tofauti ya ufanisi, kasi na gharama kati ya matumizi ya mashine za kawaida za kupulizia dawa kwa mkono na teknolojia ya kisasa ya ‘drones’.  Lengo kuu ni kuhamasisha matumizi ya teknolojia bunifu zitakazoongeza tija na ushindani katika sekta ya kilimo.

Aidha, Waziri Chongolo ameipongeza TPHPA kwa mchango wake mkubwa katika kulinda afya ya mimea, kusimamia matumizi sahihi ya viuatilifu na kuimarisha usalama wa mazao ya kilimo nchini.  Ameitaka Mamlaka hiyo kuendelea kubuni na kutumia teknolojia zinazokidhi mahitaji ya wakati na kuendana na mabadiliko ya kisayansi. 

Kuhusu utendaji kazi, Waziri Chongolo amewataka watumishi wa TPHPA kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujituma ili waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.