CHONGOLO AITAKA TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA KUANZISHA BIMA YA USHIRIKA; NA COASCO KUENDELEA NA UKAGUZI WA VYAMA
Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) zimetakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kuhakikisha ushirika unaimarika ikiwa ni pamoja na kuanzisha bima ya ushirika (COOP insurance) na ukaguzi wa maendeleo ya vyama vya ushirika.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo wakati wa kikao kazi na Taasisi hizo tarehe 24 Novemba 2025.
Waziri Chongolo amepongeza pia hatua ya TCDC kutaka kutengeneza Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Ushirika akitaka uwe wa miaka 25 kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. “Tuweke utaratibu wa kuwa na matokeo kwa hatua, kuwa mfano hadi kufikia mwaka 2030 tutekeleze tuliyojipangia kwenye Agenda 10/30 na hatimae mwaka 2050 kuwa na matokeo kwenye huo mpango kabambe tunaotaka kuutengeneza,” ameongeza Waziri Chongolo.
Kwa upande wa COASCO, imeelekezwa kutoa taarifa ya kina kila mwaka kuhusu ukaguzi wa vyama ambapo ataitolea maelekezo kuelekea kwenye mikutano ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) kwa ajili ya utekelezaji. “Ukaguzi uwe asilimia 100 na kama tatizo ni rasilimali fedha tutatafuta vyanzo ili hii kazi itekelezeke kuleta tija zaidi,” amesema Waziri Chongolo.
Kikao kazi kimehudhuriwa pia na Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo; Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu na Mha. Athumani Kilundumya, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji; wakiwemo Mrajis wa TCDC; Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo.