CHONGOLO AKAGUA MAENDELEO YA SHAMBA LA PAMOJA CHINANGALI
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ametembelea Shamba la Pamoja la Chinangali lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma tarehe 11 Machi 2026 kwa lengo la kukagua maendeleo ya uzalishaji pamoja na kusikiliza changamoto za vijana na wanawake wanufaika wa Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT).
Waziri Chongolo amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na vijana hao katika kukuza Sekta ya Kilimo, akibainisha kuwa katika msimu huu wamefanikiwa kulima jumla ya ekari 1,200 za zao la Alizeti, hatua inayochangia kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kimkakati pamoja na kuongeza kipato kwa vijana.
Aidha, Waziri Chongolo amewahakikishia vijana hao kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza ili kuweka mazingira bora ya uzalishaji, kwa lengo la kuongeza tija na kutoa hamsa kwa vijana wengi zaidi kushiriki katika kilimo chenye tija.
Kwa upande wao, vijana na wanawake wanufaika wa Programu ya BBT wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia fursa na msaada katika shughuli za kilimo, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza hamasa na matumaini ya kujenga uchumi wao kupitia Sekta ya Kilimo.
Waziri Chongolo pia amekutana na vijana wa Shambani Tour wakiongozwa na Bw. Emmanuel Mgaya, maarufu kama “Masanja Makandamizaji”, ambao walifika katika shamba la Chinangali kwa lengo la kujifunza na kujionea kwa vitendo fursa zilizopo katika Sekta ya Kilimo pamoja na umuhimu wa vijana kushiriki katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Katika ziara hiyo, Waziri Chongolo ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli pamoja na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athuman Kilundumya.