Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA KATIKA KUKUZA MAZAO YA KIMKAKATI NA KULETA TEKNOLOJIA ZA KISASA KWA WAKULIMA

Imewekwa: 06 Jan, 2026
CHONGOLO AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA KATIKA KUKUZA MAZAO YA KIMKAKATI NA KULETA TEKNOLOJIA ZA KISASA KWA WAKULIMA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amekutana na wawekezaji kutoka Kampuni ya Shandong Wanda Xing Automobile ya nchini China kujadili uwekezaji katika Sekta ya Kilimo hususan kuongeza uzalishaji wa mazao, thamani na kuleta teknolojia za kisasa zitakazoleta tija kwa wakulima.

Mkutano huo umefanyika tarehe 05 Januari 2026, jijini Dar es Salaam ambapo wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza katika mazao ya kimkakati, likiwemo zao la Korosho, kuanzia uzalishaji hadi uongezaji wa thamani wa zao hilo.  

Akieleza zaidi kuhusu majadiliano yao, Waziri Chongolo amesema kuwa wawekezaji pia wamehamasishwa kuwekeza katika uzalishaji wa mafuta ya Korosho, methanol na bidhaa nyingine.  Eneo lingine ni zao la Soya kwa ajili ya chakula cha binadamu na mifugo, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani.

Majadiliano hayo pia yalilenga kilimo cha vitunguu na uwekezaji katika mashine zinazorahisisha utengenezaji wa matuta kwa wakulima wa mpunga ili kupunguza muda na gharama za kazi shambani. 

Kwa niaba ya timu ya wawekezaji, Bw. Li Qingyu amesema uwekezaji wao utalenga kuongeza uzalishaji, kuhamisha teknolojia ya kisasa kwa wakulima, kuongeza ujuzi na kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo. 

Waziri Chongolo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje waliolenga kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha teknolojia ya kisasa katika kilimo.