CHONGOLO AZITAKA TAASISI ZA MBEGU NCHINI KUONGEZA WIGO WA UZALISHAJI, SHERIA ZAO KUSOMANA NA WATAFITI KUFIKIRIWA
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amesema katika kutekeleza malengo na mikakati iliyopangwa na Wizara na Taasisi zake, viongozi wana wajibu wa kuhakikisha kazi hizo zinaleta tija na kutatua changamoto kwa wakulima.
Waziri Chongolo ametoa rai hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI); Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) alipokutana nao tarehe 24 Novemba 2025 jijiji Dodoma.
Kuhusu TOSCI, Mhe. Waziri Chongolo ameielekeza Taasisi hiyo kuhakikisha sheria inazozisimamia kama Mamlaka, zinasomana na taasisi za TARI na ASA kwa kuwa utekelezaji wake unashabihiana. Ameitaka ASA kuongeza wigo wa uzalishaji mbegu kwa kushirikiana na Sekta Binafsi; huku akiitaka TARI kuongeza tafiti zaidi katika mazao kama kokoa na kuongeza thamani kwenye zao la ndizi kupitia nyuzi zake (fibers).
Aidha, TARI pia imeelekezwa kuwafikiria watafiti wa mbegu ili wanufaike na tafiti zao; ikiwa ni pamoja na kuongeza umri wa kustaafu kwa watafiti wabobezi ambapo watatumia utaalamu wao kujengea uwezo watafiti wengine.
Katika hatua nyingine, Waziri Chongolo ameelekeza mradi inayoendelea kutekelezwa ikamilishwe na kutoanzisha miradi mingine mipya wakati iliyopo bado haijakamilika. “Tusianzishe miradi mipya bila kuwa na matokeo yenye tija kwa miradi iliyopo,” amesema Waziri Chongolo.
Kikao kazi kimehudhuriwa pia na Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo; Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu na Mha. Athumani Kilundumya, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji; na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo.