Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO: HATUKUPI UTUKUFU USIO NA WAJIBU

Imewekwa: 15 Apr, 2026
CHONGOLO:  HATUKUPI UTUKUFU USIO NA WAJIBU

Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo waaswa kuondoa mizigo kwa viongozi na kuwajibika katika kuleta matokeo yenye tija kwa wakulima. 

“Tunapokupa dhamana ya uongozi hatukupi utukufu usio na wajibu.  Kila mmoja wenu anawajibika kuleta matokeo yenye tija kwa wakulima; na kukifanya kilimo kuwa na mvuto kwa wengine kuwekeza,” amesema Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) tarehe 14 Aprili 2026, jijini Dodoma. 

Amesisitiza Taasisi kutoa elimu kwa Umma kuhusu kazi zake, ikiwemo mifumo ya usajili na mauzo ya kilimo ili kujenga uelewa na kuimarisha zaidi utendaji wake kwa maslahi ya wakulima. 

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amewakumbusha viongozi kuhakikisha wanakabiliana na kila aina ya ubadhirifu kwa wananchi kwa kuwa ubadhirifu kidogo unaweza kuharibu taswira na kazi nzuri inayofanywa na Taasisi husika.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mweli ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kuhakikisha inatangaza kazi nzuri inayofanya kwa kuwa hatua hiyo itaongeza imani ya wananchi katika ushirika.

Kikao kazi kimehusisha Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb); Katibu Mkuu Bw. Gerald Mweli; Menejimenti ya Wizara ya Kilimo; Bodi ya Korosho Tanzania; Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika - COASCO; Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA); na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania - TCDC.