Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO: IMARISHENI UTENDAJI WA KAZI NA UBUNIFU KUENDANA NA KASI YA MAENDELEO

Imewekwa: 20 Feb, 2026
CHONGOLO:  IMARISHENI UTENDAJI WA KAZI NA UBUNIFU KUENDANA NA KASI YA MAENDELEO

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amewataka Watumishi wa Wizara ya Kilimo kuimarisha utendaji kazi na ubunifu kwa kuendana na kasi ya maendeleo kuleta matokeo yenye tija kwa wakulima. 

Waziri Chongolo amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano na Watumishi hao tarehe 19 Februari 2026 katika Ukumbi wa Viwanja vya John Malecela- Nanenane jijini Dodoma.

Amesisitiza kuzingatia taaluma, maadili na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.  Aidha, Waziri Chongolo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyompa kuiongoza Wizara ya Kilimo na kutoa wito kwa Watumishi kuwa jukumu kuu la Wizara ni kuhakikisha Taifa linakuwa na usalama wa chakula hivyo wafanye kazi kwa bidii katika kufikia lengo hilo la kitaifa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amewakaribisha Watumishi wapya na kutoa pongezi maalum kwa Bw. Joseph Kiraia kwa kulitumikia Taifa kwa uadilifu hadi alipostaafu Utumishi wa Umma. Katibu Mkuu Mweli amesisitiza kuwa Wizara ni familia inayojengwa katika misingi ya ushirikiano, uwajibikaji na nidhamu ya kazi.

Katika kuimarisha mazingira ya kazi, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kuwawezesha watumishi kwa vitendea kazi muhimu, ikiwemo vifaa vya TEHAMA vilivyokabidhiwa rasmi na Waziri kwa baadhi ya watumishi waliopokea kwa niaba ya wenzao.  Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi, tija na matumizi sahihi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Watumishi wamekumbushwa kujenga mazingira rafiki ya kazi, kuenzi mshikamano na kuheshimiana kwa kuwa ni msingi wa utendaji bora na matokeo chanya kwa wananchi.

Viongozi wengine wa Wizara walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya; Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe;; Menejimenti ya Wizara  na watumishi wa Wizara ya Kilimo.