CHONGOLO: TIJA NA BEI YENYE UHALISIA MUHIMU KWA ZAO LA PAMBA
Serikali itaendeleza jitihada za kuimarisha zao la Pamba kwa kutoa elimu na pembejeo kwa wakulima ili kuleta tija na bei yenye uhalisia kwa manufaa yao na wadau wa mnyororo mzima wa zao hilo.
Amesema Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo wakati wa Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Pamba tarehe 16 Aprili 2026, Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, Bw. Marco Mtunga, amesema kuwa zao hilo ni la kimkakati kwa uchumi wa nchi na limelengwa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni 1 ifikapo mwaka 2030. Ameeleza kuwa Bodi ya Pamba imeratibu utoaji wa huduma za Ugani kupitia programu ya BBT - Ugani Pamba ambayo imewezesha kuongeza wigo wa uzalishaji wa zao hilo ambapo katika msimu huu wa kilimo 2025/2026 tani laki 3 zinatarajiwa kuzalishwa.
Maoni mbalimbali yaliyotolewa yamejikita katika kuiomba Serikali kufanya tathmini za kina kuhusu bei ya Pamba ili imnufaishe mkulima; kuleta teknolojia za kisasa za kilimo zitakazoongeza uzalishaji wenye tija, ruzuku za viuadudu na pembejeo.
Kwa upande wa wakulima, wameiomba Serikali kuendelea kusogeza huduma za ugani karibu na wakulima na mmoja wao akieleza kuwa alianza na kilimo cha ekari moja wilayani Chato na kuvuna kilo 200 za Pamba; ambapo baada ya kuimarishwa kwa huduma za ugani amefikia uzalishaji wa kilo 2,000 kwenye hiyo ekari moja.
Washiriki kwenye Mkutano ni pamoja na Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo; Bw. Gerald Mweli, Katibu wa Mkuu wa Wizara ya Kilimo; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo; Wakulima; Wabunge na Wakuu wa Mikoa inayolima zao la Pamba; Wanaushirika; Wafanyabiashara; na Wawekezaji.