Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

CHONGOLO: TUNAENDELEA KUKUZA SEKTA YA KILIMO NCHINI KUFIKIA MALENGO TULIYOJIWEKEA

Imewekwa: 20 Nov, 2025
CHONGOLO: TUNAENDELEA KUKUZA SEKTA YA KILIMO NCHINI KUFIKIA MALENGO TULIYOJIWEKEA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Godfrey Chongolo (Mb) ameeleza kwa Menejimenti na Watumishi ya Wizara ya Kilimo kuwa kazi na malengo yaliyopangwa yatafikiwa kwa kuendeleza pale Mbunge wa Nzega Mjini, Mhe. Hussein Bashe alipoishia ili kukuza na kuleta tija kwenye Sekta ya Kilimo nchini.

Amempongeza Waziri aliyepita Mhe. Bashe, Menejimenti na Watumishi wa Wizara ya Kilimo kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele katika kubuni miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikileta tija na manufaa kwa wakulima na Taifa.

Mhe. Waziri Chongolo amesema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya ofisi na alyekuwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mbunge wa Nzega Mjini),
tarehe 18 Novemba 2025, katika Ukumbi wa Wizara, jijini Dodoma. 

Halfla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya; wakiwemo Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Kilimo zilizopo jijini Dodoma. 

Kupitia hafla hiyo, Mhe. Bashe amempongeza Waziri Chongolo kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na kumhakikishia ushirikiano wakati wowote katika kufanikisha maono makubwa ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Kilimo.