Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SERIKALI YATOA ELIMU YA MATUMIZI YA MBOLEA KWA VIONGOZI NA WANANCHI

Imewekwa: 04 Oct, 2025
SERIKALI YATOA ELIMU YA MATUMIZI YA MBOLEA KWA VIONGOZI NA WANANCHI

Katika ziara ya Wizara ya Kilimo kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Uongozi wa Wilaya ya Chunya umeomba wataalam wa kilimo kuongeza wigo wa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kutokana na kilimo kuwa ni sayansi inayohitaji matumizi sahihi ya mbolea yenye vipimo sahihi kulingana na afya ya udongo.

Rai hiyo imetolewa mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi tarehe 4 Oktoba 2025 wakati wa kikao kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya SACI Mbaraka Batenga ambaye ameeleza kuwa upimaji wa afya ya udongo ni muhimu unamwezesha mkulima kuwa na utaalam, kutumia mbolea kwa usahihi na kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Msimu wa Kilimo ulioisha mwaka 2024/2025, zao la Tumbaku limefanya vizuri, mbolea iliyosambazwa na Kampuni ya Mbolea Tanzania - TFC imeongeza uzalishaji zaidi ya makadirio yaliyokuwepo ambapo Wilaya ya Chunya, Mkoani Mbeya imezalisha tani milion 27,091.7 na kuondoa malalamiko kwa wakulima,” ameeleza SACI Batenga.

Pamoja na mafanikio hayo ameeleza kuwa bado yapo maeneo ambayo hayana mwamko wa kutumia mbolea kama eneo la kata ya Kambi Katoto na Sipa hivyo endapo watapewa elimu ya matumizi ya mbolea watahamasika kutumia mbolea na kuongeza uzalishaji.

Dkt. Nindi amepongeza juhudi za viongozi kuhakikisha wanapata mashine za kupimia afya ya udongo ili kumrahisishia mkulima kutambua aina ya udongo na mbolea inayopaswa kutumika.

Kuhusu usambazaji wa mbolea, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania - TFC, Bw. Samuel Mshote ameeleza kuwa katika msimu wa Kilimo uliopita TFC ilisambaza tani 61,000 ya mbolea ya NPK 10:18:24 kwa wakulima wa zao la Tumbaku.  Ameongeza kwa mwaka huu, TFC imepanga kusambaza takribani tani 71,000 za mbolea ya NPK 10:18:24 ambapo usambazaji wa mbolea ya NPK 10:1824 kwa Wilaya ya Chunya umefikia asilimia 85, tani 10,395 zimewafikia wakulima kati ya tani 12,230 zinazotarajiwa kusambazwa katika msimu huu.  Na kwa mbolea ya UREA na CAN tayari zipo nchini na zitaanza kusambazwa kwa wakulima ndani ya mwezi huu wa Oktoba 2025.