COASCO WAASWA KUKAGUA VYAMA VYA USHIRIKA VILETE TIJA NCHINI
Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limetakiwa kuhakikisha Vyama vyote vya Ushirika vinakaguliwa kwa wakati, huku Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ikielekezwa kuongeza kasi ya usimamizi na ufuatiliaji wa Vyama vya Ushirika nchini.
Amesema hayo Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) tarehe 6 Juni 2026 wakati akifunga Jukwaa la Tano la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Dodoma tarehe 6 Juni 2026, jijini Dodoma alimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb).
Amesema ukaguzi na uimarishwaji wa Vyama vya Ushirika nchini ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza ajira za kudumu na za muda mfupi pamoja na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, ametoa onyo kwa baadhi ya Wanaushirika wenye tabia ya kujinufaisha binafsi kwa gharama ya wanachama wengine kuacha mara moja vitendo hivyo, akieleza kuwa vinaweza kusababisha migogoro, chuki, wizi na kupoteza malengo ya msingi ya ushirika.
Naibu Waziri amesisitiza kuwa Ushirika una mchango mkubwa katika kuunganisha nguvu za pamoja, kulinda wakulima dhidi ya unyonyaji, kuchochea ubunifu na kuimarisha mafunzo ya pamoja kwa wanachama, jambo linalochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.