DKT. NINDI AHAKIKISHIA NJOMBE MBOLEA YA KUTOSHA, ASISITIZA MALENGO YA UKUAJI WA KILIMO KWA 10% IFIKAPO 2030
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen J. Nindi amewahakikishia wakulima wa Mkoa wa Njombe hakutakuwa na upungufu wa mbolea kuelekea msimu mpya wa kilimo, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa na Halmashauri zote ili kuhakikisha lengo la Serikali la kukuza Sekta ya Kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 linafikiwa.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 01 Oktoba 2025, wakati wa kikao cha tathmini ya mahitaji ya mbolea kuelekea msimu mpya wa kilimo kilichohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, Wakuu wa Wilaya za Njombe, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Bw. Joel Laurent, pamoja na Maafisa Kilimo kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe.
“Wizara ya Kilimo na taasisi zake tutaongeza juhudi kubwa kwa kushirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri. Lengo letu ni kupanua wigo wa elimu kwa wakulima na kufanya majaribio mbalimbali ili wakulima waweze kuona matokeo halisi ya teknolojia na bidhaa mpya za kilimo,” amesema Dkt. Nindi.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri umekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha wakulima wanapata elimu kuhusu bidhaa mpya za kilimo, jambo ambalo limeongeza upokeaji wa teknolojia mpya na kuonyesha haja kubwa ya bidhaa hizo, ikiwemo mbolea.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent ameeleza kuwa Mamlaka hiyo imepanga ifikapo katikati ya mwezi Oktoba 2025, tani 20,000 za mbolea zitapelekwa ili kuendana na msimu.