Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

DKT. NINDI AITAKA TARI KUHAKIKISHA TAFITI NA SAYANSI ZINAZOBUNIWA ZINAWAFIKIA WAKULIMA

Imewekwa: 04 Dec, 2025
DKT. NINDI AITAKA TARI KUHAKIKISHA TAFITI NA SAYANSI ZINAZOBUNIWA ZINAWAFIKIA WAKULIMA

Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Stephen Nindi ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kuhakikisha sayansi pamoja na tafiti za kilimo zinawafikia wakulima wote nchini ili kuwawezesha kuzitumia tenkolojia hizo kuzalisha kwa tija.

Dkt. Nindi amesema hayo tarehe 3 Desemba, 2025 katika ufunguzi wa Siku ya Udongo Duniani iliofanyika katika viwanja vya Nane Nane vya John Malecela vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma, ikiwa na Kauli mbiu “Afya Bora ya Udongo kwa Miji  Maridhawa". 

Amesema ni muhimu kuhakikisha sayansi na tafiti zinazobuniwa zinahifadhiwa kidigitali na kuwawezesha wakulima katika ngazi zote kufikia teknolojia hizo, kwa kuwa zinatoa maelezo ya kutosha kuhusu utunzaji wa udongo, matumizi ya virutubishi na mbolea pamoja na upandaji wa mazao sahihi kulingana na udongo wa eneo husika.

Dkt. Nindi amesema Wizara ya Kilimo inaendelea na zoezi la  kuhuisha ramani ya afya ya udongo nchini kupitia upimaji wa afya ya udongo kwa mizani (Scale) ya 1:50000 ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kina katika kila eneo na ikolojia zote za kilimo.

Hatua hii itawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa kila mkulima na kumuwezesha kuzalisha pasipo kuathiri afya ya udongo husika na hivyo kuzalisha kwa tija zaidi kulingana na mahitaji ya udongo.

Dkt. Nindi ameiagiza TARI kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) katika kufanya tafiti na kubaini ardhi ya kilimo pamoja na matumizi ya mifugo  ili ziweze kutambulika na kulindwa kisheria.  Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kukuza masuala ya tafiti za kilimo nchini na kuiboresha TARI ili kutoa majawabu katika Sekta ya Kilimo na kuongeza tija.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Muungano na Mazingira, Dkt. Peter Msofe; mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt.Thomas Bwana; Wakulima pamoja na Wanafunzi kutoka katika Shule ya Sekondari Nzuguni na Shule ya Sekondari ya Dodoma Sekondari.