Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

DKT. NINDI ASHIRIKI MKUTANO WA SADC

Imewekwa: 30 May, 2025
DKT. NINDI ASHIRIKI MKUTANO WA SADC

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagilaiji, Dkt. Stephen Nindi kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe ameshiriki katika Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanaoshughulikia masuala ya kilimo, usalama wa chakula, mifugo, uvuvi na ufugaji viumbemaji, tarehe 30 Mei 2025 kwa njia ya mtandao.

Majadiliano yalihusisha masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Kilimo yakiwemo; hali ya usalama wa chakula na lishe Kikanda; utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP).

Suala lingine katika majadiliano ni kuidhinisha kwa mikakati ya mazao ya mpunga na Soya katika Ukanda wa SADC na kuridhia Mpango wa Kikanda wa Uwekezaji katika kilimo (SADC Regional Agriculture Investment Plan).

Vilevile, Mkutano huo umejadili taarifa kuhusu Kituo cha Uratibu wa Utafiti na Maendeleo ya Kilimo Kusini mwa Afrika (CCARDESA) mara baada ya kutanguliwa na Mkutano wa wataalam kuanzia tarehe 26-27 Mei, 2025.

Washiriki wengine ni pamoja na Dkt. Nazael Madala aliyemwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi; pamoja na Maafisa Wandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.