Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

DKT. NINDI ATETA NA MENEJIMENTI YA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI (NIRC)

Imewekwa: 09 May, 2025
DKT. NINDI ATETA NA MENEJIMENTI YA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI (NIRC)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa juhudi inazofanya katika utekelezaji Miradi mbalimbali ya Umwagiliaji nchini.

Dkt. Nindi ametoa pongezi hizo leo Ijumaa Mei 9, 2025 alipotembelea Ofisi za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji jijini Dodoma na kufanya kikao na menejimenti ya Tume na kuwawasihi kuendelea na jitihada wanazofanya katika kuboresha sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji kwani nchi ina maeneo makubwa yanayofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji.

Ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuboresha mifumo ya uzalishaji nchini sio uzalishaji wa mazao ya kilimo pekee, bali ni pamoja na uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi, hivyo Tume ipo katikati kuhakikisha mazao yote yanazalishwa

Aidha, Dkt. Nindi amesema umuhimu wa Kilimo cha Umwagiliaji ni zaidi ya usalama wa chakula kwani matokeo yake ni kuwa na usalama wa chakula, uhuru wa chakula na kuwa na kilimo cha kibiashara ambacho kitakuza uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Sambamba na hilo, Dkt. Nindi amesisitiza Tume kushirikisha Maafisa Ardhi wa maeneo husika, ili kuepuka athari zinazoweza kutokea katika skimu kutokana na shughuli za kila siku za binadamu pamoja na kuimarisha mifumo ya kidigitali, kwa lengo la kurahisisha zoezi la ukusanyaji ada ya huduma za Umwagiliaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Bi. Maria Itembe amesema tayari Tume imeanza jitihada za kuyalinda maeneo yanayotumika kwa shughuli  za kilimo cha Umwagiliaji ili kudhibiti athari zinazoweza kuchangia uharibifu wa miundombinu na shughuli za kilimo kwa ujumla.