ELIMU YA MBOLEA YABADILI MTAZAMO WA WAKULIMA MEATU
Wakulima wilayani Meatu,Mkoa wa Simiyu wamebadili mtazamo wao hasi wa mbolea kuwa ni chanzo cha uharibifu wa udongo; ambapo wamepata elimu kuwa matumizi ya mbolea ni nyenzo muhimu ya kuuwezesha udongo kurudisha uhai wake na kuchochea uzalishaji wa mazao.
Hayo yamebainishwa wakati wa mafunzo waliyopatiwa na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na taasisi zake tarehe 04 Desemba 2025 mkoani humo katika kujiandaa na msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Newaho Mkisi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kwa kuweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo hususan mbolea na mbegu.
Bw. Mkisi amesema kuwa mahitaji ya mbolea wilayani humo yameongezeka sana tofauti na ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita. Ameeleza kuwa kwa sasa wakulima wanaelewa kuwa mbolea siyo adui wa udongo bali ni kirutubisho muhimu katika ukuaji wa mmea.
Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Godwin Vedatus, ameeleza kuwa mbolea haiharibu udongo. Kinyume chake, inauongezea virutubisho ambavyo mimea inahitaji ili kustawi kwa afya na uzalishaji wenye tija.
Aidha, mkulima Masanja Nkobadi ametoa wito kwa wakulima wenzake na kueleza kuwa “sisi Wasukuma tumekuwa tukijidanganya.
Mimi nimetumia mbolea na nimepata mavuno mengi.”