ELIMU YA MBOLEA YAWAFIKIA WAKULIMA MKOANI KATAVI
“Niwaambie vijana wenzangu - tuache dhana kwamba kilimo ni kazi ya wazee. Sasa hivi kilimo kinalipa, na Serikali imerahisisha mambo kupitia ruzuku. Ni fursa ya kizazi chetu kuamka,” amesema Bw. Maulid Macha, Mkulima kutoka kijiji cha Kasekese, mkoani Katavi tarehe 15 Oktoba 2025.
Bw. Macha ameongeza kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imebadilisha kabisa namna wanavyofanya kilimo, hasa kwa vijana wanaoanza kujikita katika kilimo. “Tunaishukuru Serikali kutuletea wataalamu wanaotufundisha kutumia mbolea kwa usahihi. Sasa napata kati ya gunia 25 hadi 30 za mahindi kwa ekari, tofauti na zamani,” ameeleza Bw. Macha.
Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wametoa mafunzo mbalimbali ya matumizi ya mbolea kwa Wakulima wa Mpunga kutoka vijiji vya Mkwajuni na Kasekese, wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambapo Wakulima wamepokea mafunzo hayo kwa kuipongeza Serikali katika kuhakikisha mbolea za ruzuku zinapatikana kwa wakati.
“Kabla ya mfumo wa ruzuku nilikuwa napata gunia kati ya 8 hadi 10 kwa ekari, lakini sasa napata kati ya gunia 20 hadi 30 za mpunga. Mbolea za ruzuku zimenisaidia sana, zamani mfuko mmoja wa mbolea tulikuwa tunanunua kwa shilingi 150,000, lakini sasa tunapata kwa shilingi 75,000 tu. Huu ni msaada mkubwa kwa mkulima,” ameeleza mkulima Bw. Bukwimba Makumucha.
Wizara ya Kilimo inaendelea kutoa elimu kwa wakulima nchini kupitia kampeni ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea” ambapo wakulima watajifunza matumizi sahihi ya mbolea, usajili wa mfumo wa ruzuku, na umuhimu wa upimaji wa afya ya udongo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua kipato.