Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

HAFLA YA KUPOKEA CHETI CHA ITHIBATI NA UBORA WA KIMATAIFA WA MAABARA YA UDONGO NA MIMEA YA TRIT

Imewekwa: 09 May, 2025
HAFLA YA KUPOKEA CHETI CHA ITHIBATI NA UBORA WA KIMATAIFA WA MAABARA YA UDONGO NA MIMEA YA TRIT

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli ameshiriki katika hafla ya kupokea Cheti cha Ithibati na Ubora wa Kimataifa wa Maabara ya Udongo na Mimea ya Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT) yenye ithibati namba  ( ISO/ICE 17025:2017) tarehe 9 Mei, 2025 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Mweli amesema kuwa upatikanaji wa Ithibati hiyo utasaidia kujenga mifumo madhubuti ya kisayansi kwa kufanya uchunguzi na uchambuzi wa mimea katika ngazi ya Kimataifa na kukuza Sekta ya  Kilimo kupitia mipango ya matumizi bora ya ardhi, matumizi sahihi ya mbolea, ushindani na kuongeza uzalishaji na mapato.

Amewataka wakulima kulima kilimo cha kisasa kwa kuzingatia matokeo ya maabara akisistiza kuwa afya ya udongo ni muhimu katika uzalishaji.  Jumla ya sampuli za udongo 8831 zinaendela kuchakatwa na kutolewa tafsiri kupitia Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania, huku Miradi mbalimbali ikiendelea ikiwemo miradi ya majaribio ya mbolea kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA).

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugezi TRIT, Bw. Jefferson Mturi amesema Ithibati hii itajenga vigezo vya ubora na kuleta imani katika tafiti zinazofanywa kimataifa.  Ameongeza kuwa TRIT itahakikisha inaleta matokeo chanya kwa wakulima kupitia tafiti bora lengo likiwa ni kukuza uzalishaji na ushindani katika Sekta ya chai.

Naye Mwakilishi wa Huduma ya Ithibati wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADCAS), Bi.Varsha Gungoa ameipongeza Serikali kwa kuweka miundombinu wezeshi ya kilimo na kupongeza upatikanaji wa ithibati katika kufanikisha mageuzi katika Sekta ya utafiti wa kilimo na uzalishaji Kimataifa.                    

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Wakurungenzi kutoka Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara; Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRIT; Wawakilishi kutoka Huduma ya Ithibati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika yaani "Southern African Development Community Accreditation" (SADCAS); Sekretarieti ya TRIT na baadhi ya Watumishi kutoka Wizara ya Kilimo.