Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

KAMATI JUMUISHI YA UENDESHAJI PROGRAMU YA TFSRP YAKUTANA PEMBA

Imewekwa: 25 Jul, 2025
KAMATI JUMUISHI YA UENDESHAJI PROGRAMU YA TFSRP YAKUTANA PEMBA

Kamati Jumuishi ya Uendeshaji wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) imekutana Mkoa wa Kusini Pemba, Wilaya ya Chakechake tarehe 24 Julai 2025 kujadili Mpango wa TFSRP.

Mwenyekiti wa kikao, Bw. Ali Khamisi Juma ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo - Zanzibar amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar mradi umejikita katika ukarabati wa miradi itakayoongeza chakula, ambapo zimetengwa hekta 8000 kwa ajili ya kuziandaa ili ziongeze uzalishaji; ambapo fedha nyingine ni kwa shughuli za kiutendaji na uendeshaji.

Amewataka wananchi kuunga mkono jitihada zinazoendelea za utekelezaji wa programu hiyo na kuwakaribisha wadau wa Sekta Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa programu ya TFSRP Zanzibar hususan katika eneo la uzalishaji mbegu ambalo lina fursa katika programu hiyo.

Naye Bw. Obadia Nyagiro, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo (aliyemwakilisha Katibu Mkuu Bw. Gerald Mweli) amesema kuwa utekelezaji wa programu ulianza mwaka 2023 huku gharama za utekelezaji zikiwa ni Dola za Marekani milioni 300; ambapo kati ya hizo, Dola za Marekani milioni 15 (Zanzibar) na Dola za Marekani milioni 285 (Tanzania Bara).

Akitoa mfano, Bw. Nyagiro amesema idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 itakuwa ni kati ya watu milioni 79 -80 na ifikapo mwaka 2050 inakadiriwa kufikia watu milioni 136 wakati ardhi haiongezeki ni ileile, hivyo uzalishaji endelevu unahitajika na wenye tija.

Ameongeza kuwa "tutahitaji teknolojia bora za kilimo  katika hatua zote za uzalishaji, ambazo zitaendana na  mabadiliko ya tabianchi.  Hii ni pamoja na miundombinu  kukarabatiwa, utafiti wa mbegu na usambazaji, huduma za ugani za kisasa ambazo Maafisa Ugani watafundishwa na kulifikisha kwa wakulima bila kusahau afya ya udongo.”